,./.,

,,

... ...

';';';';

..,,..

''=

==

\\..\\

Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Tuesday, September 20, 2016

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro 

 
By John Dotto, Mwananchi mwananchipaper@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi namna benki ya NBC tawi la Corporate ilivyopokea Sh 9,985,000 kutoka benki ya NMB tawi la Msasani na kuziingiza katika akaunti ya mteja lakini ikazitoa siku iliyofuata.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliliambia Mwananchi kuwa wanafuatilia jambo hilo kubaini mazingira hayo tata ya mteja kuingiziwa fedha lakini siku ya pili akajulishwa kupitia ujumbe mfupi wa simu kuwa zimetolewa.
“Jambo hilo lipo, lakini nawaombeni mnipe muda zaidi, kwani bado nipo kwenye uchunguzi,” alisema Kamanda Sirro.
Alipofuatwa Meneja wa NBC tawi la Corporate, Mariam Kombo ili aeleze mkasa huo alishauri mwandishi anayefuatilia sakata hilo awasiliane na Meneja Uhusiano, William Kallaghe ambaye alisema hawawezi kutoa siri za mteja wao kwa sababu maadili hayaruhusu.
Mteja wa benki hiyo aliyekumbwa na sakata hilo ni Bertha Edward Gama ambaye aliingiziwa Sh 9,985,000 katika akaunti yake iliyopo NBC tawi la Corporate jijini Dar es Salaam lakini alipotaka kuzichukua aliambiwa zimetolewa. Kwa mujibu wa Bertha fedha ziliingizwa Agosti 18 mwaka huu na zilitolewa na watu wasiojulikana Agosti 19.

Hata hivyo, benki hiyo imesema fedha hizo zinaendelea kutunzwa na benki hiyo baada ya kubaini kuwa hundi iliyotumika kuingizia fedha katika akaunti hiyo ilikuwa na dosari hivyo wao hawahusiki. Baada ya Bertha kufuatilia hatima ya fedha hizo bila mafanikio alikwenda kuripoti polisi na tayari Kamanda Sirro amesema wanafuatilia.
Mkasa ulivyokuwa

Bertha ambaye ni Ofisa Masoko wa Ema Investment Company iliyopo Mtaa wa Kitumbini katikati ya jiji aliliambia Mwananchi kuwa Agosti 17, akiwa ofisini alipokea simu kutoka kwa mteja akitaka kununua bidhaa mbalimbali kwenye kampuni yao.
Alisema mteja huyo alijitambulisha kwa jina moja la Hemed, akidai kuwa yupo mjini Morogoro na alitaka apatiwe katoni za pampers 15 na katoni 500 za tambi vyote vikiwa na thamani ya Sh 9,985,000.
Ofisa huyo alisema kuwa mteja wao huyo aliomba atumiwe namba ya akaunti ya kampuni ili aweze kuweka fedha hizo na kwamba angependa zaidi akaunti hiyo iwe ya benki ya NBC kwa sababu kampuni yake ina akaunti katika benki hiyo.

Bertha alisema walimtumia mteja huyo akaunti iliyoko Eco Bank, lakini alikataa akisisitiza apewe ya NBC ili hela ziingie haraka na yeye apate mzigo mapema. Alisema walimjibu kuwa ofisi haikuwa na akaunti NBC lakini ili wasikose fedha hizo uongozi uliamua zipitie kwenye akaunti yake iliyopo NBC tawi la Corporate.
Alisema baada ya kumtumia akaunti hiyo, saa 11.45 Agosti 18, 2016 alipokea ujumbe mfupi kutoka NBC ukisema amewekewa Sh 9,985,000 kwenye akaunti yake.

Bertha alisema baada ya kupata ujumbe huo baadaye kidogo alipigiwa simu na mteja huyo akimweleza kuwa ameshaweka fedha hizo kwenye akaunti na akasema atamtuma dereva kuchukua mzigo asubuhi ya siku iliyofuata.

Bertha alisema kesho yake asubuhi dereva aliyetumwa kuchukua mzigo alifika akachukua mzigo lakini saa 7.09 mchana alipokea ujumbe mwingine kutoka NBC ukimtaarifu kuwa fedha zimetolewa.
Alisema baada ya kupata ujumbe huu uongozi wa kampuni hiyo ulishtuka na kuamua kwenda kufuatilia kulikoni na walipofika waliripoti jinsi walivyopata taarifa ya kuingia fedha kwenye akaunti na baadaye kutolewa.

Kwa mujibu wa Bertha, benki iliwapa majibu kwa maandishi kuwa fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti yake kwa hundi kutoka benki ya NMB tawi la Msasani jijini Dar es Salaam na zilitoka katika kampuni moja (jina linahifadhiwa). Kwamba uamuzi wa NBC kuziondoa fedha hizo kwenye akaunti ya Bertha ulitokana na tofauti ya saini kwenye hundi.

Barua hiyo ya Agosti 19, 2016 ilisainiwa na Kombo ikieleza kuwa fedha hizo zimehifadhiwa na benki kama sheria zinavyotaka. Bertha alipohoji kwa nini fedha ziingie kwenye akaunti halafu ziondolewe, utaratibu wa hundi ya benki moja kwenda benki nyingine ukoje aliambiwa aandike barua ya malalamiko.
Baada ya kuandika barua na kuikabidhi benki, uongozi wa benki hiyo uliwajibu kwa barua Agosti 20, 2016 kuwa wanafanya uchunguzi na kwamba watatoa jibu baada ya siku 10.
Barua iliyosainiwa na Mkuu Huduma kwa Wateja, Ngwitika Mwakahesya inaeleza kuwa walitoa fedha hizo baada kupata taarifa kutoka Benki ya NMB ikiwaeleza kuwa hundi hiyo ilikuwa na dosari.

Benki ya NBC

Alipopigiwa simu Meneja Uhusiano, William Kallaghe ili atoe ufafanuzi alisema: “Suala hilo linahusu mteja wetu itakuwa si vema kutoa siri za mteja kwa sababu maadili hayaruhusu na pili tumepata taarifa kwamba amepeleka suala hilo polisi.”
Benki NMB. Alipofuatwa kwa ufafanuzi, Maneja wa Tawi la Msasani Mary Ngallawa alisema analifahamu suala hilo lakini hivi sasa limeshafikishwa polisi kwa hatua zaidi. “Nakuomba uende polisi unaweza kupata ufafanuzi zaidi, mimi siwezi kulizungumzia zaidi,” alisema Ngallawa.

Source:- Mwananchi Blog

0 comments:

Post a Comment

ufunguzi