,./.,

,,

... ...

';';';';

..,,..

''=

==

\\..\\

Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Wednesday, May 17, 2017

Mke wa marehemu, Zena Kassim. 
Pwani: Hali inazidi kuwa mbaya katika Wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga za Mkoa wa Pwani ambapo watu wasio na hatia wameendelea kuuawa na watu ambao hawajabainika, hivyo kufanya watu waliouawa kwa mtindo unaofanana hadi jana kufikia 22, kama kawaida yake, Uwazi limefika eneo la tukio na kuchimba zaidi.

Katika tukio hilo lililojiri usiku wa kuamkia Mei 13, mwaka huu, wauaji hao walimpiga risasi Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Bungu wilayani Kibiti, Pwani, Arife Mtulia (54), hali iliyofanya waandishi wetu kwenda kumtafuta mke wa marehemu ili kumsikia alichoshuhudia siku ya tukio hilo.
Aliyekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Bungu wilayani Kibiti, Pwani, Arife Mtulia.
MKE ASIMULIA
Akizungumza na Uwazi, jana, mke wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Zena Kassim (51), alisema kuwa, mumewe aliuawa kwa kupigwa risasi 10 na wauaji hao wakati anakwenda kuoga saa nne usiku.
“Alipigwa risasi nne mbavuni, mbili mguu wa kulia, mbili mkono wa kulia na shingoni karibu na bega risasi mbili na baada ya kumuua hawakuchukua kitu chochote,” alisema mke huyo wa marehemu huku akiwa na majonzi.

Akaongeza: “Baada ya kumpiga risasi alianguka na kwa kweli nilichanganyikiwa, ni kama nilipoteza fahamu, ni kitendo kibaya sana na cha kutisha hasa ninapovuta picha ya nilivyomshuhudia wakati anapigwa risasi.”
Alipoulizwa kama wauaji walikuwa na pikipiki au la, alisema kuwa, kwa hapo nyumbani kwake hawakufika na chombo hicho, lakini baada ya kufanya mauaji, alisikia mlio wa pikipiki, hali iliyoonesha kwamba waliiacha mbali kidogo.

Wanafamilia wakiwa msibani.
Aliongeza kuwa, anahisi wauaji walikuwa wamejificha kwenye majani na walikuwa wakimvizia kwa kuwa walioanza kuoga walikuwa ni watoto. Alisema hajui sababu ya mumewe kuuawa kikatili namna ile na watu hao kwa sababu hajawahi kugombana na mtu lakini alikuwa akipokea vitisho kila kukicha.
Alisema kuwa, mumewe alizikwa juzi Jumapili katika Kijiji cha Nyambunda na ameacha watoto tisa na mke mmoja ambaye ni yeye.

KINACHOONEKANA
Baadhi ya watu waliozungumza na Uwazi kijijini hapo jana walisema kuwa, kundi hilo la mauaji lina mawasiliano mazuri na baadhi ya wanavijiji ambao ni wasaliti ndiyo wanaowapa taarifa ya kila kinachoendelea.
“Walijuaje kuwa Mtulia alikuwa nyumbani muda huo? Mara kadhaa viongozi wamewahi kukaa vikao vya kuwajadili hawa wauaji, lakini kabla ya kikao kumalizika wanapokea meseji ya kuwaonya kwa kuwaambia kwamba wamekaa kikao kwa ajili ya wao.“Hii imetufanya tuamini kwamba, kuna wenzetu wapo sambamba na wauaji ndiyo maana wanapata habari za huku kila mara,” alisema mkazi mmoja wa eneo hilo aliyeomba hifadhi ya jina.

MLOLONGO WA MAUAJI
Habari kutoka kwa baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo ya Kibiti waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa, tangu kuanza kwa mauaji hayo ya kutisha, viongozi wamekuwa wakiuawa katika mazingira ya kutatanisha.
Staili ya watoa roho hao ni kuua kwa risasi wakitumia bunduki bila kuchukua fedha wala mali yoyote kutoka kwa marehemu husika huku wakiwa wamevalia kininja na wakitumia bodaboda, hali inayotafsirika kuwa ni mauaji ya visasi.

KWA NINI VISASI?
Juni 2014, watu wasiojulikana walivamia Kituo cha Polisi Kimanzichana na kumuua askari aliyekuwa zamu kisha kupora bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi 30.
Ilidaiwa kuwa kufuatia mauaji hayo ya askari huyo, watu 18 walikamatwa na polisi kwa uchunguzi, walihojiwa na kuachiwa huru lakini ikasemekana kuwa, nyumba yao ya ibada ilifungwa kwa amri ya serikali ikitiliwa shaka ya matumizi yake.

Ikaelezwa kuwa, baadaye viongozi mbalimbali wapatao 18 wa vijiji vya eneo hilo, walianza kupokea meseji za vitisho kutoka kwa kundi hilo la wauaji wakidai kwamba, viongozi hao waliwachongea kwa jeshi la polisi kuwa wao ndiyo waliofanya mauaji kwenye Kituo cha Polisi Kimanzichana hivyo watawaua mmoja baada ya mwingine na wakafanya hivyo na idadi ya waliotolewa roho hadi sasa imefikia 22.
Licha ya raia hao 22, polisi nao waliuawa na watu hao. Polisi hao ni Mratibu Msaidizi wa Polisi, Peter Kigugu, askari namba P.3451 Koplo Francdis, E.6990 Haruna, G.3247 Jackson, H.1872 Zacharia, H.5503 Siwale, H.7629 Maswi na H.7629 Ayoub.
Wauaji hao walipora bunduki saba, aina ya Sub-Machine Gun (SMG) nne na Long Range (LG) tatu zikiwa na risasi zake.
Jana waandishi wetu walitaka kuzungumza na viongozi wa vijiji wilayani humo, lakini hakuna aliyekuwa tayari kuzungumza wakisema, wakijulikana wanawasiliana na wanahabari, watauawa kama wenzao.

KAMANDA WA POLISI PWANI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, SACP Onesmo Lyanga alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo akisema polisi wanaendelea na uchunguzi na kwamba kama kuna mwananchi anayewafahamu wauaji hao, asisite kuwasiliana na jeshi la polisi.

0 comments:

Post a Comment

ufunguzi